Jumanne, 23 Juni 2015

Mgogoro wa Kimaslahi waibuka Machinga Comlpex, ni kuhusu deni la bilioni 31

Machinga Complex



UMOJA wa wafanyabiashara wa Soko la
Machinga Complex lililopo Ilala Jijini Dar es Salaam, wamemuomba Rais Jakaya Kikwete, kunusuru jengo hilo ili lisiuzwe na Halmashauri ya Jiji ili kufidia deni la zaidi ya Sh. Bilioni 31 linalodaiwa na mbia mwenza wa jengo hilo ambalo ni pamoja na ongezeko la riba.
Taarifa za uhakika ambazo tu imezipata na kuthibitishwa na Makamu Mwenyekiti wa wafanyabiashara hao, Gerald Mkangama, zimesema mchakato wa kuuzwa kwa jengo hilo unaendelea katika vikao vya bodi ya uendeshaji ya jengo hilo ili kupata fedha za kulipa deni hilo ambalo Halmashauri ya Jiji na mbia mwenza ambaye ni Mfuko wa Hifadhi ya Jamii wa NSSF waliokopa kwa muda wa zaidi ya miaka mitano.
Aidha, amesema licha ya ombi hilo kwa Rais Kikwete, wamebaini kwamba kuna mianya ya rushwa katika kushinikizwa kuuzwa kwa jengo hilo ambalo wamedai ni mkombozi wa maisha yao, pia katika Bodi ya Uendeshaji wa jengo hilo, pia ameitaka Manispaa ya Ilala ifungue kituo cha daladala cha Machinga Complex ili kupanua wigo wa kupata wateja zaidi.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Huduma za Soko hilo, Godwin Mmbaga, amekanusha vikali taarifa za kuwepo kwa mpango wa kuuzwa kwa majengo ya soko hilo, ili kulipa deni wanalodaiwa na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF).
Hata hivyo, amekiri kuwa siku chache zilizopita kuliibuka tuhuma za kuwepo kwa mpango wa uuzwaji wa majengo hayo, mpango ambao amedai ulikuwa umelenga kuwanufaisha viongozi wachache wenye mamlaka kwenye mauzo ya jengo hilo.
Amekaririwa akisema kuwa, anachokifahamu ni kuwepo kwa njama za kutaka aondolewe kiongozi mmoja wa bodi hiyo, njama zinazoratibiwa na kikundi cha watu wachache aliodai kuwa wanashiriki katika mpango kadhaa wa kutumia sehemu ya soko hilo kujinufaisha kwa maslahi binafsi.
“Tatizo kubwa kwenye huu mradi utasikia mambo mengi ya mimi kulaumiwa na kuambiwa sifai na kikundi kidogo cha watu ambao wanapenda rushwa. Nimekwishaweka msimamo wangu na wao wanajua msimamo wangu kwamba Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadiki, aliniteua kuwa Mwenyekiti wa DCC Business Park ili nitengeneze malengo ya kufanya mradi ule uende vizuri” alieleza Mmbaga.
Amesema wapo baadhi ya wajumbe wa Bodi ya Jengo hilo ambao wanashirikiana na baadhi ya watendaji kwenye mradi huo wa DCC Business Park kumshawishi ili aungane nao kushiriki vitendo vya rushwa huku akiapa na kuwahakikishia waliomshawishi kushiriki suala hilo kwamba ataendelea kukataa rushwa.
Uchunguzi wetu umebaini kuwa jengo hilo lililoko Ilala, Dar es Salaam linaendesha biashara ambayo hailipi na imeshindikana kulipa deni la mkopo wa ujenzi wake tangu mwaka 2012 mwanzoni na kwa muda mrefu kumekuwa na malalamiko ya Halmashauri kufanya biashara isiyolipa hivyo kusababisha ugumu wa kulipa deni hilo.
Jengo hilo la ghorofa lililojengwa na Jiji kwa lengo la kuwapatia wamachinga waliozagaa Jijini sehemu ya kufanyia biashara zao linamilikiwa na Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam na limejengwa kwa mkopo kutoka Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF).
Kwa mujibu wa taarifa kutoka ndani ya NSSF, deni la Manispaa ya Ilala na Jiji la Dar es Salaam lilikuwa halijalipwa hadi kufikia Juni 5, 2015 kama yalivyokuwa makubaliano ya awali.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni