HABARI

Uhaba wa Chakula waikumba Dodoma, Wananchi sasa waponea Ubuyu na Ukwaju

MKOA wa Dodoma umekumbwa na uhaba mkubwa wa chakula
kiasi cha familia nyingi zinazoishi mkoani humo kuanza kula vyakula vya ajabu ili kunusulu maisha yao, yakiwemo matunda ya Ubuyu.
Hali hiyo ya uhaba wa chakula katika mkoa huo, ambao ndiyo makao makuu ya Chama Tawala na Serikali yake, inaelezwa kuyakumba pia maeneo kadhaa nchini, ikiwemo mikoa ya Mtwara, Tanga na Mara.
Kutokana na hali hiyo, baadhi ya familia zilizokumbwa na njaa katika maeneo hayo yenye uhaba mkubwa wa chakula wameripotiwa kulazimika kula vyakula vya ajabu ajabu, yakiwemo majani na matunda pori ili kunusulu maisha yao wakati wakisubiri msaada wa chakula kutoka serikalini.
Lakini Bado haijafaamika na kupata takwimu rasmi kutoka mamlaka husika juu ya idadi kamili ya familia zinazokabiliwa na uhaba huo mkubwa wa chakula, lakini inakadiriwa kuwa familia nyingi kati ya hizo zinazokabiliwa na njaa katika baadhi ya mikoa hiyo, kwa takriban wiki ya tatu sasa, hazijaonja ladha ya chakula kinachokubalika kwa afya ya mwanadamu.
Hata hivyo, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, wakati wa hotuba yake ya kuahirisha Mkutano wa 13 wa Bunge la 10 mjini Dodoma mwaka juzi, alisema kwa wakati huo jumla ya halmashauri 61 nchini zilitarajiwa kukumbwa na uhaba wa chakula kutokana na tathimini ya hali ya chakula inayofanywa kila mwaka nchini.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka Dodoma, wilaya za mkoa huo zilizokumbwa na uhaba mkubwa huo wa chakula kiasi cha wananchi wake kulazimika kukimbilia kwenye ubuyu ili kupunguza makali ya njaa ni pamoja na Bahi, Kondoa, Chemba na Chamwino.
Wananchi wa Kijiji cha Suli, katika Kata ya Fufu, wilayani Chamwino, wanadaiwa kukabiliwa na njaa zaidi kiasi cha kuhitaji msaada wa haraka wa chakula cha dharura ili kuokoa maisha ya wananchi hao.
Mmoja wa wananchi wa kijiji hicho, aliyejitambulisha kwa jina la Imani Ezekel, amesema kwamba kuna hali mbaya ya uhaba wa chakula hali ambayo inawalazimu kwenda maporini kutafuta matunda ya ubuyu na ukwaju kwa ajili ya chakula.
“Tunalazimika kutumia muda mwingi maporini tukisaka Ubuyu na Ukwaju tukiwa na watoto wetu ili tuweze kupata hata unga wa uji kwa ajili ya familia zetu,” anasema Imani.
Katika Wilaya ya Chemba, kijiji kinachotajwa kuathirika pia kwa njaa kiasi cha wananchi wake kuponea matunda ya ubuyu ni Kelema Balai, sababu inayoelezwa kuchangia hali hiyo ikielezwa kuwa ni ukosefu wa mvua mwaka huu.
Mwenyekiti wa Kijiji hicho, Gwandi Kimolo, amekiri kijiji chake kukabiliwa na uhaba wa chakula, akisema tayari Serikali wilayani humo imewataka kufanya sensa ya kubaini idadi ya familia zinazohitaji msaada wa dharura wa chakula.
Mkuu wa Wilaya ya Chamwino, Farida Mgomi, amekiri wilaya yake hiyo na wilaya nyingine za Mkoa wa Dodoma kukabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula, huku akisema hali hiyo imesababishwa na mvua chache zilizonyesha mwaka huu, hivyo mazao mengi ya chakula yaliyokuwa yamepandwa na wananchi kukaukia mashambani.
Mbunge wa Jimbo la Bahi mkoani Dodoma, Omary Ahmed Badwel, amesema tatizo la njaa si katika jimbo lake tu, bali lipo kwa mkoa mzima wa Dodoma, kiasi cha baadhi yao kuanza kukimbilia maporini kusaka vyakula alivyoviita vya ajabu ili kujinusu na njaa.
Aidha, ameeleza kuwa licha ya Ofisi ya Waziri Mkuu katika kitengo kinachoshughulikia maafa kutoa tani 300 za msaada wa chakula kwa wilaya hiyo, hali bado ni mbaya kupita kiasi.
Kumbukumbu zinaonyesha kwamba tangu mwaka 2012/2013, Serikali ya Mkoa wa Dodoma ilitoa taarifa rasmi juu ya upungufu wa chakula katika baadhi ya maeneo yake kabla ya kukabidhiwa katika Ofisi ya Waziri Mkuu kwa hatua zaidi za dharura.
Mkoa wa Dodoma ni miongoni mwa mikoa ambayo iliundiwa timu ya wataalamu kutoka Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika kwa
kushirikiana na wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Kitengo cha Maafa, pamoja na wadau wengine wa maendeleo, lakini pamoja na kuundwa kwa timu hiyo, hadi sasa hakuna mabadiliko ya aina yeyote katika utendaji.
Mwanzoni mwa Mwezi Mei mwaka huu, Gazeti Mtandao hili liliripoti taarifa ya Wilaya ya Bahi kukabiliwa na njaa inayotokana na uhaba mkubwa wa chakula ulioikumba wilaya hiyo katika siku za hivi karibuni.
Kutokana na hali hiyo, baadhi ya wananchi wilayani humo waliiomba Serikali kupeleka msaada wa haraka wa chakula ili kukabiliana na hali hiyo ya upungufu mkubwa wa chakula, ombi ambalo halijatekelezwa huku familia nyingi zikizidi kuteseka kwa njaa wilayani humo.
......................................................................................................................

ZITTO KABWE KUZOMEWA TUNDUMA????



Kupitia ukurasa wa facebook wa Zitto Kabwe aliandika hiki
 

"Kuna watu wanasambaza video kuwa eti nimezomewa Tunduma. Sijawahi kufanya mkutano wowote wa kisiasa Mjini Tunduma. Ni wanasiasa uchwara tu ndio wanaweza kujitekenya na kucheka wenyewe. Mwenye picha au video yenye kunionyesha dhahiri kuwa nilikuwa Tunduma aweke hadharani. 

Siasa za kuzusha uongo hazitaivusha nchi hii. Waliotumwa kufanya kazi hiyo wanawadanganya waliowatuma. Sisi tunaendelea kufyeka mapori"


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni