SIKU chache baada ya kuripoti taarifa juu ya
hatari ya kutokea machafuko makubwa ya kisiasa katika Wilaya ya Kyerwa, Mkoa wa Kagera, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimezinduka na kutoa onyo kali kwa baadhi ya wafuasi wa vyama vya upinzani nchini wanaojihusisha na vitendo vinavyotishia uvunjifu wa amani.
Hivi karibuni Gazeti Mtandao hili iliripoti kuwepo kwa baadhi ya wananchi katika wilaya hiyo wanaodaiwa kuwa wafuasi wa baadhi ya vyama vya siasa nchini, wanaoendesha vitendo vya kihalifu na uvunjifu wa amani, vikiwemo vya kufyeka mazao mashambani pamoja na kuchoma moto nyumba na maduka ya baadhi ya wananchi kwa sababu za kisiasa.
Kwa sasa Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana yuko katika ziara ya kukagua uhai na kuimarisha chama hicho mkoani Kagera, ziara ambayo imemfikisha katika Wilaya ya Kyerwa, ambako vitendo hivyo vya uvunjifu wa amani vimekuwa vikifanyika kwa kisingizio cha siasa.
Kutokana na hali hiyo, chama hicho kimetoa onyo kwa baadhi ya wafuasi wa vyama vya upinzani kuachana na vitendo hivyo, huku kikiagiza vyombo vya dola kuwachukulia hatua za kisheria wote watakaobainika kuhusika na vitendo hivyo vya uhalifu na vitisho kwa wananchi.
Akizungumza akiwa katika ziara ya Katibu Mkuu huyo wilayani humo, Katibu wa NEC (Itikadi na Uenezi), Nape Nauye, amesema mwishoni mwa wiki iliyopita chama chake kimewaonya wanachama na wafuasi wa vyama hivyo vya upinzani kupitia mkutano wa hadhara, akisema vitisho hivyo walifanyiwa wananchi 'walioonyesha nia ya kupigia kura vyama wanavyovitaka nje ya Ukawa'.
Kwa mujibu wa Nape,vitendo hivyo vilivyofanywa na baadhi ya wafuasi wa vyama vya siasa nchini, kwa kuchoma moto makazi ya watu, maduka na kuharibu mazao mashambani, haviwezi kuvumiliwa na Serikali inayoongozwa na CCM akidai kwamba vitendo hivyo ni kinyume cha sheria na vinatishia amani na utulivu wa nchi.
Aidha, amesema pamoja na CCM kuviagiza vyombo vya dola kuchukua hatua dhidi ya wahusika, lakini kuanzia sasa wanachama na wafuasi wa Chama Tawala hicho hawatakuwa tayari kuona wakiharibiwa mali zao, na badala yake watakabiliana kwa nguvu zote na vitisho hivyo.
Uchunguzi wa awali ulibainika kwamba vitendo hivyo vilichochewa na Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, uliofanyika Desemba mwaka jana, ukiwahusisha wenyeviti wa vijiji, mitaa na vitongoji.
Maeneo yaliyodaiwa kuathirika zaidi na vitendo hivyo vya kiharifu, vingi ya vitendo hivyo vikiwakumba viongozi wa vijiji ni pamoja na Kata za Mabira, Kaitambuzi na Katera, huku ikielezwa kuwa familia nane zilikuwa zimekumbwa na kadhia hiyo katika maeneo hayo kwa kuachwa bila makazi baada ya nyumba zao kuchomwa moto huku pia zikiwa zinakabiliwa na njaa baada ya mazao yao mashambani kufyekwa.
Vyanzo vyetu kadhaa vya habari hizi kutoka wilayani humo, vinasema chanzo cha matukio hayo ya uhalifu ni hasira walizonazo baadhi ya wananchi wanaodaiwa kuwa wafuasi wa Chadema, ambao wagombea wao wa nafasi mbalimbali za wenyeviti wa vijiji, vitongoji na mitaa, waliwekewa pingamizi na wagombea wa CCM, hivyo kuwafanya wagombea hao wa Chama Tawala kupita bila kupingwa.